MTANDAO wa Wanafunzi Nchini (TSNP) umemuunga mkono Rais John Magufuli
kwa kuwachukulia hatua za kuwawajibisha waliohusika kuwadahili
wanafunzi wasio na sifa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Aidha, mtandao huo umeishauri serikali kusitisha programu maalumu ya
kusomesha walimu wa masomo ya sayansi ili kutoa fursa kwa wanafunzi
waliodahiliwa kumaliza masomo yao na pia serikali kupanga utaratibu
mpya.
TSNP pia imeiomba serikali kuwaruhusu wanafunzi ambao wamebakiza
mwaka mmoja wa kumaliza masomo yao ya Stashahada (Diploma) waendelee na
masomo yao. Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa mtandao huo, Alphonce
Lusako katika mkutano wa kutoa tamko la mtandao huo pamoja na la
wanafunzi waliofukuzwa UDOM.
Lusako alisema, hatua hiyo haiepukiki kutokana na wahusika kudahili
kinyume na vigezo vilivyowekwa na serikali. Aidha, alisema mtandao huo
ulikuwa ukifanya utafiti wa kina kupitia Idara ya Tafiti na Mafunzo ya
mtandao huo kuhusu sakata hilo.
Alisema serikali ilianzisha programu hiyo kwa lengo la kutatua uhaba
wa walimu wa masomo ya sayansi na kuwekwa sifa za udahili, lakini
hatimaye Waziri mwenye mamlaka aliondoa na kuongeza kuwa ikitokea
mwanafunzi au kundi la wanafunzi halitapewa haki zao, mtandao huo
utashirikiana na wadau wa elimu zikiwemo Asasi za kiraia kufungua kesi
mahakamani ili kudai haki zao.
Akisoma taarifa rasmi ya wanafunzi waliosimamishwa UDOM, Gibson
Johnson alisema, wanaiomba serikali kuangalia uwezekano wa wao kuendelea
na masomo yao.
“Tunaiomba na kuililia serikali iangalie wale wenye division I, II na
III ituache tumalizie masomo yetu, lakini watakaokuwa na ufaulu wa
chini kuanzia division IV itafute namna ya kuwasaidia,” alisema Johnson.
Wamemuomba Rais Magufuli na Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuona haja ya kuwarudisha
chuoni ili kumaliza masomo yao kama ilivyopangwa, kama jambo hilo
likishindikana serikali ifanye mkakati wa kuwatafutia vyuo stahiki ili
wamalize masomo yao.
Post your Comment



