MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameomba boti za kivita
kutoka nchini China ili kusaidia ulinzi katika ukanda wa bahari ya
Hindi.
Aliomba boti hizo Dar es Salaam jana wakati alipotembelea boti ya
Jeshi la Wanamaji kutoka China waliokuja nchini kwa ziara ya kirafiki
wakiwa wametoka kutekeleza jukumu la kushiriki katika ulinzi katika
Ghuba ya Aden.
Alisema upatikanaji wa boti hizo utasaidia kudhibiti wanaoingiza na
kushusha mizigo kwa njia wa magendo sambamba na wanaovamia watu na
kupora mali za watu katika fukwe hapa nchini.
Makonda alisema kuna nyumba zilizo kama maghala ambayo hayafunguliwi
mchana, yanaingiza mizigo usiku na kuisababishia serikali hasara kwa
kutoingiza kodi, hivyo boti hizo zitakazokuwa za kisasa zitakuwa msaada
mkubwa kwa Polisi katika Kanda ya Dar es Salaam, kufanya ukaguzi katika
ukanda wa bahari ya Hindi.
“Naomba mtusaidie boti kama tatu au nne ambazo tunaamini zitasaidia
kuimarisha ulinzi, na kuhakikisha vitendo vya uhalifu katika bahari
unatoweka kabisa,” alisisitiza.
Alisema pia serikali ya mkoa imezungumza na Balozi wa China nchini
kuhusu kuanzishwa kwa kituo kitakachofundisha polisi 300 watakaokuwa na
uwezo wa kufika sehemu yoyote ya mkoa linapotokea tukio ndani ya dakika
tano.
Alisema kuanza kwa mpango huo mkoa utakuwa wa kwanza kwa Bara la
Afrika kuwa na askari wa aina hiyo, hivyo serikali ina wajibu wa
kulishughulikia na kufanikisha mchakato huo kwa askari wa nchi kavu na
hata majini.
Mkuu wa Tawi la Mipango la Maendeleo Jeshini, Meja Jenerali Simon
Mumwi alisema ziara hiyo itawasaidia kubadilishana uzoefu na wanamaji
kutoka nchini kwao na taarifa mbalimbali huku akiahidi kudhibiti wa
matukio ya kihalifu, hasa katika ukanda wa bahari.
“Niseme tu bahari yetu ni salama na jeshi la wanamaji lipo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi,” alisema Mumwi.Balozi wa China nchini, Lu Youqing alisema ujio wa meli hiyo ni
ishara ya njema ya mwendelezo wa ushirikiano mzuri kati ya China na
Tanzania uliodumu tangu enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere.
Post your Comment



