MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa wiki mbili kwa
wakuu wote wa wilaya mkoani kwake, kuhakikisha wanatengeneza mpango
kazi, utakaowezesha kuwatumikia wananchi.
Makonda alitoa agizo hilo jana wakati akiwaapisha wakuu hao,
walioteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo. Alisema kutengenezwa na kukamilika kwa mpango kazi huo katika kila wilaya, kutawasaidia kutengeneza pia wa mkoa.
“Someni vizuri ilani ya Chama Cha Mapinduzi na ahadi zote za mwaka
2015/2020, pitieni hotuba ya Rais ambayo iliainisha vipaumbele vyote.
Someni mazingira ya kazi katika maeneo yote mliyopewa kwenda kuwatumikia
wananchi mkifanya hivyo tunaamini tutaweza kuja kutengeneza mpango kazi
wa mkoa,” alisema Makonda.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kila baada ya siku 90 wakuu hao wa
wilaya, watakuwa wakijieleza kwa wananchi kuhusu kazi walizopewa katika
maeneo yao na kwamba atakayeshindwa, atafutiwe wilaya nyingine.
Alisema shughuli hiyo, itakuwa ikifanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu
Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Wakati huo huo ametoa wiki moja kwa
wakuu hao wa wilaya, kuhakikisha maeneo yote ambayo yalikuwa yakifanya
biashara za shisha, yamefungwa.
“Shisha imekuwa tatizo hapa nchini. Nataka mlifanyie kazi kwa uzito
zaidi suala hili kila mtu ahakikishe hakuna biashara ya shisha katika
wilaya yake,” alisisitiza Makonda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuapishwa , wakuu hao wa
wilaya, wamesema watahakikisha wanafanya kazi zao za kuwatumikia
wananchi kwa weledi.
Walimuahidi mkuu wa mkoa kutimiza yote aliyowaagiza wafanikishe
kutengeneza Dar es Salaam mpya. Akizungumzia vipaumbele atakavyosimamia
wilayani kwake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alitaja ujenzi wa
barabara zenye ubora na udhibiti wa ombaomba.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgadilwa alisema kipaumbele
kikubwa atakachoanza nacho ni kushughulikia ugawaji wa wilaya hiyo,
ikiwemo kubaki kwa madiwani na vyanzo vya mapato na kuitangaza wilaya
hiyo ili wananchi waitambue.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felex Lyaviva alisema ili kukabiliana na
rushwa ambayo ni changamoto nchini , ataanzisha vikundi mbalimbali
ikiwemo vikundi vya akinamama na vijana wananchi wawe na shughuli ya
kufanya kuondoa mianya ya rushwa.
“Rushwa ni tamaa wapo wafanyakazi wanaoona ni sehemu ya maisha yao
bila kuomba rushwa hawawezi kufanya kazi. Nitatoa namba yangu kwa
mwananchi yeyote atakayeombwa rushwa awasiliane na mimi, lazima vitendo
hivi tuviondoe,” alisema
Post your Comment



