VIKOSI vya uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma,
vinaendelea na kazi ya kuwasaka abiria tisa, kati ya 45, waliozama maji
baada ya kutokea kwa ajali ya boti katika Ziwa Nyasa juzi.
Hadi sasa watu 36 wameripotiwa kuokolewa kutokana na kazi kubwa,
iliyofanywa na vikosi vya uokoaji vya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana
na wananchi wanaoishi katika vijiji vya pembezoni mwa Ziwa Nyasa.
Chanzo cha habari kutoka eneo la tukio,kilisema
kuwa boti hiyo ilizama baada ya kugonga mwamba ndani ya ziwa hilo saa
tisa alasiri jirani na kilipo kijiji cha Mkenda wilaya ya Nyasa mkoani
Ruvuma.
“Ni kwamba boti ilikuwa na jumla ya abiria 45, lakini hadi sasa ni
abiria 36 ndio waliookolewa wakiwa hai na wengine tisa bado
hawajajulikana mahala walipo.Ilikuwa ikitokea katika kijiji cha Nakawale kuelekea kijiji cha Mitomoni.
“Ni vigumu sana kwa sasa kusema kama hao ambao hawajapatikana
wamekufa maji au la, maana inawezekana wakawepo ambao baada ya kujiokoa
walikimbia na kutokomea kusikojulikana kutokana na kiwewe,” kilisema
chanzo hicho.
Kwa mujibu wa mashuhuda, abiria waliookolewa katika ajali hiyo
walifikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma na kupatiwa matibabu na
baadaye kuruhusiwa kwenda makwao kutokana na afya zao kutengamaa.
Habari zaidi kutoka eneo hilo la tukio, zilisema kuwa nahodha wa boti
hiyo, Said Auyu alitokomea mahali kusikojulikana baada ya kujiokoa
katika ajali hiyo.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma,
Zuberi Mwombeji ili kuzungumzia tukio hilo kwa kina hazikuweza
kupatikana kutokana na kile kilichooelezwa na wasaidizi wake kuwa
alikuwa katika eneo la tukio, kufuatilia kazi ya kuwaokoa abiria ambao
bado hawajapatikana.
“Hivi unavyozungumza na mimi, RPC (Mwombeji) amerudi tena katika eneo
la tukio ili kuongeza nguvu ya kuwatafuta abiria tisa waliosalia na
baada ya kukamilisha kazi hiyo atakuwa katika nafasi nzuri ya kuwapa
taarifa za kina za ajali hiyo,” alisema mmoja wa wasaidizi wa RPC,
ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake.
Post your Comment



