Get the latest updates from us for free

mas template
Home » , , » Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 02

Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 02

Written By Bigie on Friday, February 23, 2018 | 6:29:00 PM

Mwandishi: Grace Godfrey Rweyemam

Mume wangu ni hodari sana wa kuonyesha mapenzi na ingawa hufuata kwa umakini masharti yake kwamba mimi nisionekane kama mke wa tajiri, lakini kiukweli alinionyesha mapenzi ya dhati. Alinisifia na kunisaidia hadi kazi za ndani kwani hakutaka tuishi na binti wa kazi. 

Tulikuwa na wafanyakazi wawili waliokuja na kuondoka ila mara kadhaa aliwaambia wasije wapumzike. Naweza kuhesabu ni mara ngapi nimepika kwani mara nyingi sana mume wangu hupika, hufua mpaka nguo zangu za ndani, na hata kuniogesha. 

Watoto wakiwa katika umri wa kuhudumiwa na mzazi mara zote yeye ndiye huwahudumia, bila shida yoyote, yaani hata kuamka usiku. Mwanzoni nilikuwa naona ni vitu vya ajabu au labda anafanya hivyo kunisahaulisha alichoniambia lakini mpaka leo hii ni mwaka wetu wa sita na hajabadilika, kiasi cha kunifanya mimi niwe mvivu wa kazi.

Nilipoendelea kuishi naye nilianza kugundua vitu vya ajabu, na wewe ni mtu wa kwanza kabisa ninakwambia. Sijui kwanini nimeamua kukutafuta nikwambie, na sielewi ni wapi nimepata ujasiri mkuu namna hii, lakini nikifuatilia ushuhuda wako, nilianza kushawishika kuwa unaweza kunisaidia. Sitaweza kukueleza kwa kirefu kuhusiana na uchawi wa mume wangu, lakini kwa kifupi ni mchawi mkubwa sana hapa nchini. 

Huua watu wengi na ameshawaua hata wazazi wake mwenyewe, na ninavyokwambia sio kwamba nimehadithiwa bali yeye mwenyewe amewahi kukiri kwa kinywa chake kuwa ndiye aliyeua wazazi wake. 

Nyumbani kwangu nimeshakutana na vitu vingi vya ajabu. Ninavyokwambia, nimeshawahi kuona kwa macho yangu damu na nyama za watu kwenye frij yake maalumu nyumbani ambayo alinizuia kuigusa, halafu siku moja akasahau funguo. 

Nakumbuka siku hiyo nilikua bado sijapata uhakika kuwe yeye ni mchawi kwani hakuwa amekiri, bali nilihisi tu, sasa siku aliposahau funguo ya hiyo friji ambayo kuna chumba ameiweka, kiherehere changu nikaenda kuifungua, kidogo nizimie. Si rahiri uamini Grace vitu nilivyoviona nab ado nikaendelea kuishi na yule mwanaume. Mule kulikuwa na nyama za watu, kwa sekunde chache nilizosimama nimeduwaa mbele ya hilo jokofu, niliona hadi mikono ya watoto.

Mume wangu anawapenda sana watoto wetu, lakini juzi kati nimejiona nikiwa usingizini kama tuna nyang’anyana naye mwanangu wa pili, mwenye umri wa miaka miwili, huku nikimlilia asimuue. Kilichoniogopesha, asubuhi niliamka nikamuhadithia, hata hakuonesha kujali kabisa hiyo ndoto. Sasa kwa kuwa namjua nilipata mawazo sana, nikahisi anataka kuua na watoto wetu. Hiyo imepelekea ugomvi mkubwa sana kati yetu, nikimshutumu kuwa atawaua na watoto wetu, huku namuahidi kumuacha. Ukweli ni kwamba natamani sana nimuache huyu mwanaume, lakini siwezi kabisa. 

Nimewaza mara nyingi mno kumuacha lakini siyo tu kwamba ananitishia kuwa sitaweza kuendelea kuishi tukiachana, bali ni kama ameukamata moyo wangu kiasi cha kushindwa kabisa kufanya maamuzi. Ninampenda kuliko kitu au mtu yeyote duniani, na najua haya si mapenzi ya kawaida. Kila nikijilazimisha kumuwazia ubaya, nafsi yangu ni kama inamtetea, najikuta nakumbuka na kutafakari mema yake tu. 

Najua ubaya wake mwingi na najua ni mtu hatari sana ninaishi naye, pia najua jinsi gani watoto wangu na hata ndugu zangu wako katika hatari kwa mimi kuwa kwenye hii ndoa, ila sina jinsi ya kujitoa. Huyu mwanaume ameteka fahamu zangu kwa asilimia mia moja. Huwezi amini nitakachokwambia, mimi na mume wangu hatuwezi kupitisha siku moja bila kufanya tendo la ndoa, na ni mimi ndio huhitaji hata zaidi yake. 

Akisafiri basi inatulazimu kutumia teknolojia ya mtandao kujiridhisha kwani mwili wangu hauwezi kukaa siku moja bila tendo la ndoa na huyu mwanaume. Najijua nimefanywa mtumwa, lakini moyo wangu unampenda kupita kiasi na siwezi kabisa kumuacha.

Kilichonisukuma kutafuta msaada wa haraka ni hofu ya kumpoteza mwanangu. Baada tu ya kile nilichokiona katika ndoto, na huo ugomvi mkubwa kutokea kati yetu, amekuwa akinihakikishia kuwa hakuna namna ninaweza kumuacha, hata akinifanyia tukio la kuniumiza sana. Ninaongea naye nalia sana halafu yeye mwenyewe ndio ananibembeleza kwa maneno ya mahaba na kisha tunafanya tendo la ndoa, kila siku usiku. 

Asubuhi naanza tena kumlaumu na kumwambia hofu yangu, huku nikilia kwa wasiwasi wa kumpoteza mtoto wangu. Naumia kwamba hakanushi kuwa hana mpango wa kumuua mtoto, ingawa hakubaliani, badala yake hunipooza tu na kunitaka maisha yaendelee. 

Hakuna mtu anaweza kuelewa namna ninavyojisikia hata nikitoa maelezo gani. Pia mtu huweza kudhani haya mambo ni ya kufikirika, hata ningekua mimi ningedhani hivyo kwani sikuwa naamini mambo ya uchawi, lakini ni kweli haya ndiyo maisha yangu. Naishi na shetani, ninayejua ni shetani, lakini nampenda kuliko binadamu yeyote chini ya jua.” Alimaliza kunieleza binti huyo, nikiwa namtazama kana kwamba naangalia muvi ya ajabu.

Kwa miaka yangu ishirini na mbili katika ukristo, nimekua nikisikia kuwa kuna wachawi na kusikia shuhuda kadhaa za kichawi, lakini sikuwa nimewahi kukutana na simulizi la ana kwa ana toka kwa mchawi mwenyewe au mtu anayeishi na mchawi kama mume. 

Mara nyingi mimi huwa si mtu ninayestushwa sana na visa vya maisha ya watu. Yaani mtu anaweza kuniambia mambo yake au siri zake za ndani kabisa, za kushangaza, lakini nikamsikiliza kana kwamba nilikua nazijua kabla. 

Nimejifunza kuwa hakuna jipya chini ya jua, hata kama ni jipya masikioni mwangu. Hii imenisaidia kuwa mshauri mzuri kwa watu wenye mizigo mizito, kwani huwa nasikiliza bila kupaniki na nina uwezo wa kumshauri mtu akili ikiwa imetulia.

Nikimsikiliza Jovina, sikuonyesha kabisa kushangazwa na alichokuwa akinihadithia, lakini kiukweli ndani ya nafsi yangu nilishikwa na mshangao mkubwa. Alichozungumza hakikuonekana kuwa na ufumbuzi akilini mwangu kabisa. 

Nilijiuliza maswali kadhaa wakati nikiendelea kumsikiliza ambayo sikuyapatia majibu. Nilijiuliza msaada anaoutegemea kwangu kama anaweza kuupata hata nusu yake, sikupata jibu. Mimi ni mzuri katika kutoa ushauri, na pia kutoa msaada wa kiroho kwa njia ya maombi. 

Kikawaida nikimuahidi mtu nitamuombea kuhusiana na jambo lake, huwa lazima nimuombee. Mara nyingi Mungu ameweka mzigo ndani yangu kuwabeba watu kwa maombi, na huwa nafanya hivyo kwa kadiri niwezavyo. Lakini huyu binti alihitaji msaada zaidi ya ambao nina uwezo wa kumpa.

 ITAENDELEA
#TrueStory

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya