MWANAMKE mmoja anashikiliwa na polisi wilayani Bunda, mkoani Mara kwa
tuhuma ya kumuua mtoto wake kwa kipigo, baada ya kumtuhumu kumuibia Sh
8,000.
Kamanda wa polisi mkoani Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi Ramadhan
Ngazi juzi alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo, lililotokea majira ya
saa 11:30 jioni katika mtaa wa majengo eneo la Bunda Day mjini hapa.
Pili Omondo (28), mkazi wa mtaa huo alimpiga kwa fimbo kichwani mtoto
wake ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Kabarimu na
kumsababishia kifo.
Alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Wakuru Rungu (9) na kwamba baada ya
kipigo hicho alimbeba na kumpeleka hospitalini, akidai kwamba amegongwa
na pikipiki na ndipo muda mfupi akapoteza maisha. Kamanda Ngazi alisema
kuwa mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa na polisi na upelelezi ukikamilika
atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma ya mauaji ya mwanawe.
Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa mwanamke huyo alimpiga mtoto
wake kwa kumgongesha kichwa ukutani akidai ni mwizi sugu na kwamba
baadhi ya majirani walipomzuia alidai kwamba hata kama akimuua ni
mwanawe.
Katika tukio lingine, mwanamke mmoja ambaye hajafahamika jina wala
makazi yake amejifungua kichanga na kukitupa pembezoni mwa barabara kuu
ya Mwanza-Musoma, katika eneo la mtaa wa Balili mjini hapa.
Post your Comment



