Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshiriki katika Mkutano wa Masuala ya Afya wa Mawaziri unaoandaliwa na Chuo Kikuu cha Harvard ujulikanao kama Harvard Health Leaders' Ministerial Roundtable uliofanyika Geneva leo.
Mkutano
huo wenye lengo la kujenga uwezo wa Mawaziri wa Afya na Wataalam kwa
njia ya kubadilishana uzoefu umehudhuriwa na mawaziri wa Afya kutoka
nchi zaidi ya 40 wakiwemo Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud
Thabit Kombo.
Katika
Mkutano huo, Mheshimiwa Rais Mstaafu alialikwa kushiriki na kuelezea
uzoefu wake katika mjadala kuhusu 'Mafanikio ya Kukumbukwa kwa Kuwezesha
Utekelezaji wenye Matokeo' (Achieving a Legacy in Goverment by Getting
Things Done).
Katika mjadala huo,Rais
Mstaafu Kikwete alielezea uzoefu wake kuhusu changamoto za utekelezaji
wa programu na miradi ya Serikali na chimbuko la kuanzishwa kwa 'Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa' (BRN) ikiwemo mafanikio na changamoto zake.
Katika jopo hilo, walishiriki pia Mhe. Baroness Tessa Jowel, Waziri wa
Zamani wa Uingereza wa Masuala ya Olimpiki na Waziri wa Utamaduni,
Michezo na Habari, na Mheshimiwa Idris Jala, Waziri katika Ofisi ya
Waziri Mkuu wa Malaysia anayeshughulikia Mpango wa Ufuatiliaji wa
Utekelezaji wa Programu na Matokeo Malaysia ujulikanao kama PEMANDU.
Mheshimiwa
Rais Mstaafu ameelezea changamoto aliyoipata kabla ya kuansishwa kwa
BRN ambapo ilikuwa vigumu kujua na kufuatilia kwa uhakika hatua
inayopigwa katika utekelezaji wa miradi na shughuli za Serikali. Kiu
yake ilipata jawabu alipofanya ziara nchini Malaysia na kujifunza namna
Mpango wao wa PEMANDU ulivyokuwa ukifanya kazi.
Aliamua kujifunza kuwaalika wataalamu wa PEMANDU kuja kusaidia wataalam wa Tanzania kubuni mpango wa BRN.
Ameusifia mpango wa BRN kuwa umewezesha ufanisi kwa kuwezesha kupata 'matokeo makubwa kwa rasilimali zile zile'.
Aidha
mpango umewaleta pamoja wadau wote wa ndani na nje ya Serikali
kushirikiana pamoja na kuainisha changamoto, kukubaliana vipaumbele,
ufumbuzi, kugawana majukumu na kuhimizana katika kutimiza wajibu wa kila
mdau. Aidha imewezesha kuwepo kwa takwimu na uwazi katika uendeshaji wa
shughuli za Serikali na uwajibikaji wa Serikali katika kutekeleza ahadi
zake. Pamoja na uzuri wa mpango huo na mafanikio yaliyopatikana,
changamoto kubwa ilikuwa ni upatikanaji wa rasilimali katika kutekeleza
miradi hiyo kwa wakati.
Katika
mjadala huo, Mawaziri wa nchi za Afrika wamevutiwa na uzoefu wa
Tanzania na Mpango wa BRN na wameonyesha shauku ya kutaka kujifunza
zaidi juu ya mpango wa BRN. Wamempongeza Rais Mstaafu Kikwete kwa
kuonyesha uongozi kwa kuwezesha ubunifu katika utekelezaji wa programu
za Serikali ambao umekuwa na matokeo mazuri yenye kupimika.
Rais
Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akifafanua jambo katika
Mkutano wa Masuala ya Afya wa Mawaziri unaoandaliwa na Chuo Kikuu cha
Harvard ujulikanao kama Harvard Health Leaders' Ministerial Roundtable
uliofanyika Geneva leo. Wengine ni Mhe. Baroness Tessa Jowel, Waziri wa
Zamani wa Uingereza wa Masuala ya Olimpiki na Waziri wa Utamaduni,
Michezo na Habari, na Mheshimiwa Idris Jala, Waziri katika Ofisi ya
Waziri Mkuu wa Malaysia anayeshughulikia Mpango wa Ufuatiliaji wa
Utekelezaji wa Programu na Matokeo Malaysia ujulikanao kama PEMANDU.
Rais
Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Waziri wa Afya
Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwenye mkutano huo. Kushoto ni Waziri wa Afya
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo.
Balozi Modest Melo akiwa na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo mkutanoni
Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo.
Post your Comment


