Get the latest updates from us for free

mas template
Home » , » Kabla Sijafa - Sehemu ya 02( Simulizi ya Kweli)

Kabla Sijafa - Sehemu ya 02( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie on Friday, March 2, 2018 | 10:18:00 AM

Mwandishi: Grace G. Rweyemam
“Ninaandika wosia huu siku chache kabla ya kifo changu, ikiwa ni njia pekee ninayoweza kuonyesha ni jinsi gani nisingependa kilichonitokea kimtokee mtu mwingine yeyote. Kwa kila atakayebahatika kusoma, naomba ajue kwamba nimeandika kwa lengo la kumsaidia kujua kuwa humu duniani tunapita, na hata kama unadhani unamiliki dunia, ipo siku utaiacha. Ninafariki nikiwa na miaka 40, ninamuacha mke na watoto wangu wawili ambao bado wananihitaji sana kama baba. 

Ninamuua mke wangu na kumkatishia ndoto zake, mwanamke msomi na mwerevu sana. Siwezi kumlaumu kwa lolote, ingawa mwanzoni nilihisi kama ni sahihi kutoka nje ya ndoa aliponiudhi kidogo au sana. Sasa najiuliza, ni mara ngapi yeye nilimkosea ila hakutoka nje ya ndoa. Uzinzi ni kama kulamba sega la asali, na ukishaanza kamwe si rahisi uache.

Mara ya kwanza kabisa kutoka nje ya ndoa ni wakati ndoa yetu ikiwa na miaka mitatu. Nakumbuka siku moja mke wangu alikuwa amenuna. Sikumbuki ni sababu gani hasa ilimfanya anune, ila nakumbuka mara kadhaa alininunia endapo ningemuudhi. 

Tabia ya kununa iliniudhi sana, ingawa hakuninyima chakula wala kuacha kufanya majukumu yake. Kilichoniudhi zaidi ni vile ambavyo nilitumia nguvu nyingi kumfanya anipe haki yangu ya tendo la ndoa. Mwanzoni aliponuna, nilijitahidi kumbembeleza na kujipendekeza, baada ya muda akawa sawa. Lakini siku zilivyosogea, nilikuwa nikikereka sana akininunia, hivyo hata kama ningekuwa na kosa, ningejifutia na badala yake kumuhesabia yeye kosa.

Siku hiyo aliponinunia, niliamua nitaondoka nyumbani na kwenda sehemu yoyote ile bila kumuaga. Mida ya saa mbili na nusu usiku nilitoka, siku ya ijumaa, nikaenda kwenye baa moja, haikuwa mbali sana na maeneo tuliyoishi. Mimi si mnywaji kabisa, hivyo niliagiza maji tu nikawa nakunywa. Ghafla alinishika bega mtu, nikageuka na kuona ni mwanadada tunayefanya naye kazi ofisi moja, serikalini.

 Alidai kuwa alikuja hapo kununua kiti moto, akaniona nimekaa peke yangu, akaona aje anisalimie. Alisogeza kiti na kukaa, akaanza kunidodosa kwanini niko hapo na huonekana mwenye mawazo. Kama kuna kosa nilifanya siku ile ni kumwambia ukweli kuwa tuna mgogoro na mke wangu na kumueleza kiundani kuhusiana na tabia ya mke wangu kuninunia. 

Yule binti alionesha kunihurumia sana, akanifariji, tukazungumza kama masaa mawili au matatu. Nilirudi nyumbani nafsi ikiwa imechangamka, halafu nikachukua ushauri wa yule dada kwamba akinuna namie ninune mpaka nitakapoona amerudi hali ya uchangamfu tena.

Hayo yalianza kuwa maisha yetu kuanzia kipindi hicho. Tulinuniana hata siku mbili, tatu au hata wiki. Mimi niliendelea na maisha, nikawa karibu na yule dada tuliyefanya naye kazi, na sasa kwa kuwa tayari alijua kuhusu mke wangu, mara zote tukiwa tumenuniana, nilimwambia ukweli. 

Alitumia fursa hiyo kunifariji na kunifanya nisijihisi upweke hata kama hatuzungumzi na mke wangu. Thamani ya mke wangu kwangu ilianza kupungua kwani huyu binti alinifanya nione kuwa anayepoteza ni mwanamke na siyo mimi. 

Hatukuweza tena kufanya tendo la ndoa kila mara tuliponuniana, na ni kama huyu binti wa ofisini alijua, akawa akijaribu kuniweka karibu au hata kunitaka tukale chakula cha jioni pamoja. Kwangu niliona ni fursa, kwani nilikusudia kumkomoa mke wangu kwa kutokula hata chakula chake endapo ameninunia.

Mara nilianza mahusiano ya mapenzi na yule dada wa ofisini, jeuri yangu kwa mke wangu ikaongezeka sana, kwani sasa niliona kuna mwanamke mwingine wa kuniridhisha, tena wakati wowote ninaotaka. 

Tuliendelea na mahusiano moto moto na yule binti kwa muda wa miezi mitatu, halafu siku moja nikapigiwa simu na mwanaume mwenzangu akinionya niachane na mke wake vinginevyo angeniharibia kwa mke wangu. Kiukweli sikuwa tayari mke wangu ajue au aniache, hivyo ule mkwara niliuogopa. 

Nilimuuliza yule binti kuhusu hiyo simu, akajibu kuwa ni kweli ana mpenzi na wana malengo ya kuoana, na kwa bahati mbaya amekuta mawasiliano yetu, hivyo akaamua kunitafuta. Nafsi yangu iliuma kana kwamba ni mke wangu kanifanyia hivyo. 

Yule dada alidai kuwa yuko tayari tuendelee, ila akawa akidai nimpatie pesa, yaani akaanza kunifanya kama buzi. Mishahara yetu haikuwa inatofautiana sana na mimi nilikuwa na majukumu, nikaanza kuhisi ni kama anataka kunifanya kulipia tendo la ndoa toka kwake, nikakereka na kumuacha. Hapo nikawa nimepoteza faraja yangu, hivyo mke wangu akawa akininunia napata shida sana. Niliamua ni bora nitafute mwanamke mwingine ambaye hatakuwa na mtu, awe faraja yangu.

Ndani ya miezi michache tu, nilipata mtu mwingine, binti wa chuo kikuu wa mwaka wa kwanza, tukaanza mahusiano, nikiamini nitakuwa peke yangu. Tulikaa kwenye mahusiano, nikawa tayari kumuhudumia kwa gharama ndogondogo, ili asiwe na tamaa. 

Miezi mitano ya mahusiano, niligundua kuwa yule binti anatoka na pedeshee mmoja. Na nilipomuuliza alikiri huku akinishangaa kuwa nilidhani kwa vihela vyangu hivyo ningekuwa peke yangu? Nilianza kuhisi kuwa kumbe wanawake nje ya ndoa si waaminifu, nikaamua nitatafuta mke wa mtu, nikiamini kuwa nikibahatika akanikubali basi nitakuwa peke yangu. 

Nilipata mke wa mtu kweli, tukaanza mahusiano yenye mapenzi tele. Huku kwangu mke wangu aligundua kuwa siku hizi mimi si mwaminifu tena, ingawa hakuwa na uthibitisho. 

Hali ya ndani ilizidi kuwa mbaya, nikawa naona jinsi ninavyomtesa lakini sijali. Tuliendelea na mapenzi yetu na huyo mke wa mtu, nikamuona ananifaa kweli, kwani alijua mapenzi kuliko wote niliokuwa nao kabla, akiwemo na mke wangu. 

Tulikaa mwaka mzima, tukipendana na hakuna aliyemuumiza mwenzake. Baada ya mwaka, mumewe ilitokea akajua kuhusu mahusiano yetu, akawa akinitafuta.

ITAENDELEA KESHO
#TrueStory

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya