Mwandishi: Grace G. Rweyemam
Yule muhubiri aliendelea kushuhudia, “Mwaka mmoja baadaye, nikiendelea kuomba na kumsihi Mungu aniponye, Mungu alinifundisha kuwa ninacho hitaji sio uponyaji, kwani huu mwili unapita na kuna siku nitauacha, hata kama nimekamilika kimaumbile, nilifundishwa kuwa ninachohitaji ni kuliishi kusudi la Mungu kwenye maisha yangu.
Roho mtakatifu alianza kunifundisha kama mkristo, ninatakiwa kufanya nini hasa, na hapo ndipo nikaelewa kuwa sababu kubwa ya Yesu kuja duniani haikuwa kuponya, bali kuokoa wenye dhambi. Nikiwa bado ni kiziwi na bubu, nilianza kufikiri njia sahihi ya kuwambia watu kuwa Yesu anawapenda, na kwamba waache dhambi zao na kumgeukia Muumba wao. Nilimshirikisha mama jambo hilo, akafurahi na kuanza kunisaidia kufanya hivyo kwa njia iliyokuwa rahisi kwangu.
Nikiwa na miaka 19, nilianza kuhubiri injili katika shule za watu wasiosikia, kwa kutumia lugha ya ishara, lakini pia kwa kuwa nilijua kusoma na kuandika, niliandika mahubiri, mama akanisaidia kuchapisha na tukaanza kuwasambazia watu.
Nafsi yangu ilianza kuwa na amani sana kwa kile nilichokifanya, nikagundua hilo ni jambo jema zaidi kwenye maisha yangu. Siku moja nikiwa katika kuhubiri shule fulani ya watu wasiosikia, kijana mmoja alitoka nje na kufunga mlango kwa nguvu, nikasikia sauti ya mlango kwa ukubwa sana, nikastuka. Sikuamini kuwa ni kweli nimesikia sauti ile ya mlango, nikapuuza na kuendelea kuhubiri, halafu muda mfupi nikasikia tena sauti ya upepo mkali, nikastuka na kuangalia nje.
Nilikatisha mahubiri haraka na kuondoka, kwani sikuelewa nini kinaendelea. Nilipoingia kwenye gari, dereva wetu aliweka mziki, na kwa mara ya kwanza kabisa nikasikia sauti ya mziki ikipiga kwenye redio ya gari, na huo ndio ukawa uponyaji wangu.”
Siku hiyo baada ya ibada nilijiona kama mama asiyewajibika kabisa. Nilijilaumu kwa kumkatia tamaa binti yangu na kuona kama ndio kapoteza kesho yake. Nilijilaumu kwa kuwa dhaifu kiasi hicho, kiasi cha kushindwa kuomba ipasavyo kwa ajili ya mwanangu, kiasi cha kushindwa kuona wema wa Mungu eti sababu mtoto kaugua.
Nilirudi nyumbani, nikamuacha Karitta na baba yake sebuleni, nikaingia chumbani, na haya ndiyo maombi niliyoomba siku hiyo, “BWANA wangu, naomba unisamehe kwa kushindwa kujua nafasi yangu kama mama kwa maisha ya binti yangu Karitta.
Nisamehe kwa manung’uniko na huzuni iliyopitiliza kiasi cha kutoona upendo wako kwetu. Kama isingekuwa mkono wako, Karitta wangu angeshakufa, lakini pia kuna mema mengi mno umetenda kwenye maisha yangu na ndoa yangu, nina sababu ya kukushukuru. Najua ugonjwa wa Karitta siyo kazi yako, ni kazi ya adui, lakini najua Wewe bado ni mwema. Wewe ni nguvu yangu ninapokuwa dhaifu, tena U Mungu mpiganaji wangu siku zote, na nina hakika unasikia nikuombapo.
Leo hii naomba juu ya mwanangu kwa mara hii tena. Nimekuomba umponye mara nyingi sana, lakini sasa nataka jambo jingine toka kwako. Kwa kipindi ambacho atakuwa bado hajapona, naomba unisaidie kuwa mama bora kwake. Nisimuhurumie kupita kiasi na kumfanya ashindwe kuliishi kusudi lako kwenye maisha yake.
Ni kusudi lako asome, hivyo niwezeshe kumsaidia asome. Pia niwezeshe kumsaidia kucheza na kujichanganya na wenzake. Niwezeshe hata kumsaidia kujifunza Neno lako, na kuuona upendo wako katika hali yoyote aliyonayo.”
Kuanzia siku hiyo, hiyo ndiyo ilikuwa aina ya maombi yangu. Nilitumia muda mwingi zaidi kuomba na kutafakari Neno, nikaanza kuona Mungu akinipa amani ndani ya nafsi yangu. Huzuni ndani yangu ilianza kupungua, nikagundua kitu, kwamba kwa kadiri nilivyokuwa na amani ndivyo na Karitta alianza kuwa mchangamfu. Ghafla nikaona furaha na amani ya mume wangu pia inaanza kurudi, na hali ya familia ikaanza kuboreka kwa maana ya kwamba ile hali ya kukosa tumaini ndani yetu ikatoweka.
Nilifatilia shule ambayo angeweza kusoma, lakini badae nikaona ni vema nikimtafutia mwalimu aje kuwa anamfundisha nyumbani, na labda kumpeleka shule za kawaida ili ajichanganye na watoto wenye akili za kawaida.
Nilianza kuamini kumuacha kwenye mikono ya dada aliyenisaidia kumlea, kwani nilijua Mungu yupo kumlinda mahali popote hata kama mimi sipo. Siku zilisogea, Karitta akaanza kuwa na uchangamfu, akaweza kuwa anakaa, ingawa bado hakuwa anajitegemea. Taratibu nilianza pia kuona akili yake ikirudi kawaida na uelewa wake ukiongezeka. Hii ilinitia moyo, na sasa mbali na kuwa alifundishwa na mwalimu, mimi binafsi nilianza pia kumfundisha.
Nilisoma naye Neno la Mungu bila kujali anaelewa au la, nikawa nikiona akinitazama na kucheka kila nilipojaribu kumuelewesha. Tulianza kuwa na wakati mzuri zaidi na mwanangu, kwani alinionyesha kupokea yale niliyomfanyia au niliyozungumza naye, kwa kucheka. Hakuwa na uwezo kabisa wa kuongea, lakini niliamini kuna siku atazungumza.
Tofauti na awali ambapo nilimhesabia kama mtoto asiye na akili timamu tena, asiyeweza kufanya chochote wala kuelewa chochote, sasa nilimchukulia kwa asilimia kubwa kama watoto wengine, isipokuwa mwenye kasoro kidogo. Sikuruhusu akili yangu ione mapungufu na udhaifu wake, bali nililazimisha kuona nguvu yake.
Niliamua kuwa nitazungumza naye maneno ya kumjenga na kumtia moyo, na kumfundisha kuhusu upendo wa Mungu. Hapa naweza kufananisha na mtu apandaye mbegu ya mti ambao huchukua miezi kadhaa kwa mbegu hiyo kuota na huchukua miaka kadhaa kutoa matunda.
Miezi ilivyosogea, mbegu niliyokuwa nikiipanda kwa Karitta kweli ilianza kuota taratibu. Uzima ndani yake ulianza kuonekana, na ule uso au muonekano wa kitaahira ukaondoka. Mate yaliyomtoka mara zote, yalipungua na hadi kuisha kabisa, na aliweza kukaa kwa kujitegemea, akawa akianza sasa kusimama na hatimaye kutembea.
Nakumbuka siku moja nikiwa naongea naye, namfundisha na ninamchekesha kama mtu tunayeelewana vizuri, alirudia neno nililouwa nimesema, “nguvu.” Lilikuwa ni neno la kwanza kabisa kumsikia mwanangu akilisema, tangu ameanza kuugua.
Nilimsaidia arudie tena neno hilo lakini hakurudia tena na wala hakusema tena, badala yake akaendelea kucheka tu. Kwangu mimi kutamka lile neno moja tu niliona kama wingu kama kiganja cha mkono, na nilijua kabisa hiyo ni dalili njema sana ya mwanangu kuzungumza.
Niliongeza muda wa kuongea naye, na baba yake akawa akifanya hivyo pia. Tulimjengea mazingira ya kuwa tunaongea na kumpa nafasi ya yeye kuongea, yaani tukawa hatumfanyi kama mtu asiyeweza kuongea. Tulizungumza naye, tukimuonyesha kuwa tunatarajia naye azungumze, kwa namna mbalimbali kama kumuuliza maswali, au kumhamasisha aseme.
Hilo zoezi lilifanyika kwa miezi mitatu mizima bila kurudia kusema chochote, kiasi cha kutukatisha tamaa tena, lakini nikaiambia nafsi yangu kuwa lazima kuna siku Karitta wangu ataongea tena, na atazungumza vizuri kabisa.
ITAENDELEA
#TrueStory
#TrueStory
Post your Comment