Get the latest updates from us for free

mas template
Home » , » Nguvu ya Dhaifu - Sehemu ya 04 ( Simulizi ya Kweli)

Nguvu ya Dhaifu - Sehemu ya 04 ( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie on Saturday, March 10, 2018 | 2:03:00 PM

Mwandishi: Grace G. Rweyemam

Siku moja wakiwa wanacheza na pacha wake, ambaye naye nilimfundisha kuishi na ndugu yake akitaraji kuwa kuna siku atakuwa mzima tena, na kucheza naye kama mtu mwenye akili japo kwa uangalifu, mimi nikiwa jikoni napika, alikimbia Kareen jikoni akipiga kelele kuwa Karitta ameita mama. Nilimbishia Kareen, halafu nikajistukia kuwa kwanini nambishia mtoto wakati hilo ni jambo tumekuwa tukimuomba Mungu na kuamini kuwa litatokea. 

Nilienda sebuleni na kujaribu kumuhamasisha Karitta aite tena, huku nikiwa sina matumaini kwani mara ya kwanza alisema mara moja tu na hakuwa amerudia tena mpaka baada ya miezi mitatu. Cha kunishangaza, aliita tea, “mama” kabla hata sijamlazimisha muda mrefu. Huwezi elewa furaha niliyoipata siku ile. Nilitoa machozi ya msisimko. Niliona kama Mungu amenijibu kwa haraka kuliko niilivyotarajia. Nafsi yangu iliinuka kwa upya, Imani yangu kwa Mungu ikaongezeka.

Karitta alianza kutamka neno moja moja kuanzia wakati huo, tukaanza kumfundisha kusema kama ambavyo mtoto hufundishwa. Kareen alinipa ushirikiano mkubwa katika kumsaidia dada yake, kipindi hicho wakiwa na miaka sita kuelekea saba. Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu baadaye, mwanangu aliweza kuzungumza vizuri, ingawa si kwa haraka, na hakujua maneno yote, lakini kwangu huo ulikuwa muujiza mkubwa sana. 

Pia aliweza kutembea mwenyewe, kwani tulimuanzishia mazoezi ya kutembea, kabla hata hajaanza kusema, na namshukuru Mungu miguu ilikaza na akaweza kutembea vizuri. Mpaka sasa, ni miaka saba imepita tangu binti yangu augue, lakini ugonjwa wake umebaki ni ushuhuda. Kwa muonekano hana tena tofauti na watoto wengine, na ingawa amezidiwa maradasa mawili na pacha wake, lakini anafanya vizuri sana darasani na amerudi kwenye uchangamfu wake wa awali.

Zaidi sana, katika kipindi kigumu sana nilichopitia cha kumuuguza mwanangu, nimejifunza kuwa mama ni nini hasa. Wengi tunatamani kuwa na watoto mara tu tuingiapo kwenye ndoa zetu. Na wengine huthubutu kutaka watoto hata pasipo kuwa na ndoa. Mara kadhaa tumewauliza, au kuwazungumza kwa pembeni au hata kuwahurumia wale wasio na watoto. Imeonekana kama ni sheria kila mtu kuwa na mtoto maadamu ameoa au ameolewa. 

Vijana wa sikuhizi wameona fahari kuzalisha, na wamefurahia kuwaweka watoto wao kwenye mitandao ya kijamii na kujisifia juu yao. Jambo moja wengi wetu hatulijui, kwamba watoto sio tu zawadi inayotolewa na Mungu, bali pia ni jukumu. Mungu anapokupa mtoto, uwe baba au mama yake, hakupi tu kiumbe, bali hukupa nafsi hai. Hakuna mtengenezaji wa gari anayetengeneza gari zuri asijue ni kwanini amelitengeneza. Trekta limetengenezwa kwa ajili ya kufanya kazi za shambani kama kulima na kupalilia, na ni kulikosea heshima yake ikiwa utanunua trekta ulitumie kuendea ofisini.

Mungu anapokupatia mtoto, anajua na kusudi la kumuumba huyo, na anatarajia wewe mzazi umsaidie kuishi sawa na ambavyo Muumba wake anataka. Kuna wazazi wengi tutaulizwa habari za watoto wetu mbele ya haki tusiwe na cha kujibu. 

Tunawekeza katika kuwafurahisha watoto, tunawekeza katika kuwapa elimu bora, yote ni mema kabisa, lakini ni misingi gani tunaitengeneza kwa ajili ya maisha yao ya kiroho? Ni kiasi gani tunawalea watoto ili waje kuwa wake na waume bora kwa wenzi wao? Ni namna gani tunawasaidia kuwa na tabia zinazokubalika katika jamii? Sijui kama umewahi kufikiri endapo utakufa ghafla, mwanao akiwa umri wa miaka 12, 13 au chini ya hapo, au umri wowote wa kulelewa, je ataishi na watu na kupendwa? 

Ni rahisi kumwambia binti wa kazi afanye kila kitu kwa ajili ya mwanao, na ukafurahi kuwa mtoto anapata muda mzuri wa kucheza, kusoma na kuangalia katuni, lakini kumbuka kuwa huyo mtoto akilelewa na mtu mwingine kitakachomfanya apendwe sio katuni na elimu, bali tabia njema na maadili.

Leo hii tumekuwa wazazi ambao muda pekee tunaowapa watoto wetu ni siku za wikiendi kwenda nao ufukweni. Hatuna muda wa kujua mambo ya ndani ya watoto wetu, hatuna muda kuchunguza na kujua siri za mioyo yao. Wengine tumethubutu kuwapeleka shule za bweni wakiwa katika umri mdogo, na hatuna habari nini hasa kinaendelea wakiwa huko mashuleni. 

Tunatengeneza kizazi kisichojua umuhimu wa mahusiano na familia kwa kuwapa watoto simu katika umri mdogo, na kuwaruhsu kuwa bize na mitandao ya kijamii, michezo ya kompyuta, katuni na vipindi vya televisheni. 

Hatuna muda wa kufanya ibada na watoto wetu, hatuna muda wa kuwa na mazungumzo ya kifamilia, kutaniana na kucheka wakiwepo, hatuna hata muda kukaa nao kwa ukaribu na kujenga urafiki nao, na tunadhani kwa kuwambia tu tunawapenda na kuwanunulia wanachohitaji tutawaonyesha upendo.

Watoto wengi wametafsiri upendo wa mzazi kama kupewa kila anachotaka kwa mzazi, jambo ambalo si sahihi hata kidogo. Hatuwapi nafasi kujifunza kuwa kuna wakati dunia itakupa mahitaji yako ila kuna wakati itakunyima. Hatuwapi fursa ya kuona kuwa kuna sababu njema ya kutopata kila unachotaka. Tunajenga kizazi kisichojua kujitafutia, kizazi kisicho na uvumilivu wa maisha na kizazi kisichojua maana halisi ya upendo. 

Tunadhani katika umri mdogo watoto hawaelewi maisha ni nini, bila kujua chini ya miaka mitano ndio umri ambao mtoto hujifunza maana halisi ya maisha. Kila ninapomuangalia Karitta wangu, simuoni kama tu mtoto, namuona ni mtumishi mkubwa wa Mungu ambaye Mungu amenipa fursa kubwa ya kumsimamisha katika misingi impasayo. Lakini hii haimfanyi kuwa bora kuliko Kareen kwa namna yoyote ile. Endapo nitashindwa kumsaidia Kareen kuelewa kuwa thamani yake ni sawa kabisa na ya pacha wake, ingawa yeye hakuumwa, nina cha kujibu pia mbele za Mungu.

Kwa sababu tofauti, kuna wazazi wameonyesha upendeleo kwa watoto wao wengine dhidi ya wenzao hivyo kuwasabishia watoto chuki kati yao. Wamewafanya watoto wakue katika kutojiamini na hivyo kutoonyesha karama au thamani zilizo ndani yao sababu tu wenzao wameonekana bora kuliko wao. Kila mtoto ni tofauti na mwenzake. Mmoja kuwa na kipaji fulani kinachoonekana haimfanyi kuwa bora kuliko yule ambaye huenda mpaka anakua hujajua kipaji chake. 

Wengine vipaji vyao vimesitirika, ila vinahitaji kujengewa kujiamini zaidi ili vionekane. Hata akili za darasani ni tofauti kwa kila mtoto, lakini mwingine akipaliliwa vizuri huwa bora katika eneo fulani na atang’aa kama nyota katika eneo hilo. 

Hakuna mtoto yeyote anayepaswa kuonekana bora kuliko mwenzake, kwani hakuna mtoto aliyepatikana kwa bahati mbaya. Kila mmoja, hangezaliwa endapo Mungu asingekuwa na kusudi naye. 

Haijalishi ni mtoto wa kiume wa pekee, wa kike wa mwisho au vyovyote vile, kama mzazi, daima usimfanye mtoto kuwa bora kuliko mwenzake au wenzake kwa namna yoyote ile. Huo ni mwiba unaupanda, na utakuja kukua na kukuchoma wewe mwenyewe, pamoja na watu wengine.

Ni vema kila mzazi ajifunze, na hili ndio ombi langu kubwa kwako mzazi na mzazi mtarajiwa. Jifunze kuwa baba, jifunze kuwa mama. Mama sio tu yule aliyebeba mimba miezi tisa na kuzaa, wala baba siye yule tu aliyempa mimba mwanamke na kumzalisha. 

Kuwa mzazi ni kuwajibika, kuwajibika kwa mahitaji ya mwanao kama ambavyo sote hufanya, lakini zaidi sana kuwajibika kwa tabia za mwanao. Mfanye mtoto wako kuwa mke mwema wa mtu atakayemuoa, au mume mwema kwa mwanamke fulani. Mfanye pia kuwa baba au mama bora kwa atakaowazaa. 

Anza jitihada za makusudi za kutengeneza watu sahihi katika jamii yetu. Ifanye jamii kuwa mahali salama zaidi kwa kuanza kuwekeza katika tabia za mtoto au watoto ambao Mungu anakupa neema ya kuwa mama au baba kwao. 

Usifanye haraka kutaka kuwa na mtoto, ukiona fahari tu ya kuanza kuitwa baba au mama mapema, eti sababu umri unasogea basi utafute tu kuzaa. Watoto au mtoto unayetaka kumzaa anahitaji upendo wa baba na mama yake kwa usahihi. Usimnyime haki ya kuwa na wazazi wake wote wawili kwa haraka ya kuzaa (vinginevyo labda Mungu aamue kumnyima kulelewa na mzazi/wazazi).

Na mwisho ninawashukuru nyote mliofatilia na kujifunza kutokana na simulizi langu.

MWISHO...

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts